Friday 29 May 2015

MTOTO AFARIKI BAADA YA KUTUMBUKIA KWENYE SHIMO LA CHOO

Mtoto mmoja Reuben Daud(3) mkazi wa Nyihogo wilayani Kahama mkoani Shinyanga amefariki dunia leo baada ya kutumbukia kwenye karo la choo ambapo mazingira ya tukio hilo hayakufahamika.



Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema mnamo saa 3 ya asubuhi kulizagaa taarifa ya kupotea kwa mtoto katika eneo hilo na ndipo jitihada za kumtafuta zikafanyika na kumkuta akielea kwenye karo la choo nyumba ya jirani amefariki.

Mmoja wa mashuhuda hao Khalfan Mohamed ameelezea tukio hilo kuwa alisikia taarifa za kupotea kwa mtoto ambapo baadae taarifa za kupatikana kwa mtoto huyo akiwa ameelea kwenye karo, hivyo taratibu za kuuopoa mwili zikafanyika. 

Kwa upande wa baba mzazi wa mtoto huyo Daud Reuben ameelezea tukio hilo kuwa mtoto aliondoka kwenda kununua kitafunwa kwa ajili ya chai lakini hakurudi ndipo walipowashirikisha majirani kumtafuta ambapo walimuona kwenye karo hilo akiwa amefariki.

Naye mtendaji wa mtaa huo Simon Mabumba amesema uzembe wa kuacha makaro wazi ndiyo chanzo cha matukio kama hayo kuendelea kujitokeza hivyo wananchi wanapotaka kujenga wanapaswa kuzingatia usalama wa jamii na si kuangalia shughuli zao tu. 

Jeshi la Polisi wilayani Kahama lilifika katika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu na kisha kuupeleka chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya ya Kahama kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!