Monday 2 March 2015

SERIKALI KUUGAWA MKOA WA MBEYA

Serikali imeyapokea maombi ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mbeya (RCC) yanayopendekeza mkoa huo ugawanywe na kuwa miwili ya Mbeya na Songwe.

Akizungumza na maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Chunya kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi katika uwanja wa Saba saba, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Serikali imeridhia maombi hayo kutokana na ukubwa wa mkoa huo ambao una kilometa za mraba 63,000.
“Tumekwishapokea maombi ya kuugawanya Mkoa wa Mbeya kwa sababu una eneo la kilometa za mraba 63,617 zilizogawanyika katika wilaya 8 na halmashauri 10. Hili ni eneo kubwa sana kiutawala, siyo rahisi kuusimamia na kusukuma mbele maendeleo,” alisema Pinda.
Alisema kamati hiyo imeshauri mkoa huo ugawanywe katika wilaya nne, huku akifafanua kuwa mkoa mpya wa Songwe utakuwa na wilaya za Ileje, Momba, Mbozi na Chunya. “Wamekubaliana makao makuu yatakuwa Mbozi lakini ninyi wa Chunya mmeenda mbali zaidi kwa kuigawa Chunya kwenye wilaya mbili za Songwe na Chunya itaenda Mbeya,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
Alisema katika kikao hicho ilikubaliwa kwamba makao makuu ya Wilaya mpya ya Songwe yatakuwa Mkwajuni.
Mkoa wa Mbeya una wilaya nane zilizogawanyika katika tarafa 27, kata 262, vijiji 842 na mitaa 252. Idadi ya wakazi kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni 2,707,410.
Akizungumzia kuhusu mpango wa maji katika wilaya hiyo, Pinda alisema bado kuna changamoto kubwa ya kuyafikisha vijijini. “Tuna mpango wa kuchimba visima vikubwa vitatu na mwakani tuna mpango wa kuchimba visima vingine virefu 11, tunachohitaji ni fedha na usimamizi,” alisema.
Alivitaja vijiji vitakavyonufaika kuwa ni Makongorosi, Mkwajuni, Kapalala, Isangawana, Galula, Lupa na Matwiga. Vingine ni Kambikatoto, Tanile, Bitimanyanga na Mapogoro.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amezindua maabara tatu katika Shule ya Sekondari Saza zilijengwa kwa ufadhili wa Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Shanta.
Akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbuli alisema ujenzi wa maabara hizo tatu umegharimu Sh268.5 milioni.
ikijumuisha pia ununuzi wa samani, uwekaji wa mfumo wa maji na gesi.
“Kati ya hizo Sh 23.5 milioni ni za ununuzi wa vifaa vya maabara na kemikali na Sh245 milioni ni ujenzi wa jengo, samani na uwekaji wa mfumo wa maji na gesi,” alisema.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Mbozi ambapo mbali ya kuzungumza na wananchi, atazindua maabara Vwawa sekondari, atakagua ghala la nafaka la NFRA na kupokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji wa miche ya kahawa kwenye kituo cha TACRI - Mbimba

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!