Monday 2 March 2015

FAHAMU JINSI YA KUKABILIANA NA HOFU KUFIKIA MAFANIKIO



Fahamu jinsi ya kukabiliana na hofu ili kufikia mafanikio
Kuna mambo mbalimbali yanayowakwaza baadhi ya watu katika kufikia mafanikio ili waweze kuishi maisha wanayoyataka wao.


Hata hivyo, pamoja na kuwepo vikwazo mbalimbali hivyo, kipo kikwazo kimoja ambacho ndicho hasa adui mkubwa wa binadamu katika kuyafikia mafanikio anayoyataka. Kikwazo hicho ni hofu.
Hofu inasababisha wasiwasi, msongo wa mawazo na kumwondoa binadamu kwenye furaha. Tofauti kubwa kati ya watu waliofanikiwa na wale ambao hawajafanikiwa, inaanzia hapo kwenye hofu.

Hata hivyo, si kwamba watu waliofanikiwa hawana hofu yoyote, la hasha! Hofu wanayo, lakini wanajua jinsi ya kukabiliana nayo. Kwa upande mwingine, watu ambao hawajafanikiwa, wamefikishwa hapo kwa sababu wanakubali hofu iongoze maisha yao.

Watu ambao hawajafanikiwa, wanapoingiwa na hofu tu, basi wanaacha kabisa kuendelea kufanya kile ambacho walitaka kukifanya na kuanza upya jambo jingine.

Katika makala haya, nawaalika wasomaji wa FikraPevu tujadili jinsi mtu anavyoweza kukabiliana na hofu. Hofu ni nini? Kwa maelezo rahisi, hofu ni hisia zisizo nzuri juu ya kitu, mtu au jambo fulani. Hisia hizo humpeleka mtu kuamini kwamba mbele yake kuna hatari, hasara au kuumia.

Hofu inaweza ikawa na matokeo ya kweli au isiwe na matokeo yoyote. Mtu anatengeneza hofu yake kwenye akili yake. Mara nyingi vitu ambavyo watu wanahofia, vinakuwa havijatokea bado, ingawa wanajaribu kutengeneza picha fulani ya kitu ambacho kinajengewa mazingira akilini kwamba endapo kitatokea itakuwaje.

Kwa mfano, mtu anaweza akawa na wazo la kuanzisha biashara zake, lakini akawa na hofu kwamba biashara hiyo itamtia hasara. Biashara hajaianza, hasara hajaipata, lakini anajengwa tayari picha kwamba kuna uwezekano wa kupata hasara.

Sehemu kubwa ya hofu zinazowazuia watu kuchukua hatua, ni hofu za kujitengenezea wenyewe kwenye akili zao. Hofu za aina hii, huweza kupata nguvu hasa pale mazingira yanapodhibitisha hofu hizo. Kwa mfano, kwa mtu anayetaka kuanzisha biashara, lakini akaanza kuhofia kupata hasara, atajielekeza kuwaangalia wafanyabiashara walioshindwa kuendeleza biashara zao, wale waliopata hasara.

Njia zifuatazo zinaweza kutumika kukabiliana na hofu za aina hiyo
Ili kuondokana na hofu, mtu anahitaji kujijengea tabia ya ujasiri. Uzuri ni kwamba tabia ya ujasiri, mtu anaweza kujifunza kama ambavyo anaweza kujifunza kitu chochote. Mtu anaweza kujijengea ujasiri kwa kubadili mtazamo wake wa mawazo.

Kwa mfano, mtu anapaswa kufahamu kuwa katika kila malengo anayojipangia atakutana na changamoto mbele yake, na pale zinapomtokea changamoto hizo, anatakiwa kujipa ujasiri na kutambua kwamba changamoto hizo haziwezi kuwa kikomo cha yeye kuendelea na malengo yake.
Kwa kutambua tu kwamba katika mipango na malengo yake mtu huyo atakutana na changamoto, na kisha akatambua kwamba pindi atakapozivuka changamoto zote hizo, atayafikia malengo yake, hapo lazima ujasiri uwepo kwa ajili ya kupambana na hofu ya aina yoyote.
Kutambua chanzo cha hofu
Njia nyingine ya kuweza kuondokana na hofu husika ni kutambua chanzo chake. Tatizo la hofu ni kwamba huwa si jambo au kitu halisi. Ni ni picha tu ambayo mtu anaijenga katika akili yake.

Mara nyingi hofu nyingine anajengewa mtu tangu utotoni mwake kwa kuambiwa na ama wazazi wake au wakubwa zake kwamba hana uwezo wa kufanya hiki wala kile. Kwa hiyo kwa kujengwa hofu ya aina hiyo, hata pale mtu anapojaribu kufanya jambo lile aliloambiwa hawezi halafu akakutana na kizingiti, taswira ile ya hofu inaanza kuja akilini kwamba haiwezekani kweli na hivyo kukata tamaa mapema.

Ni lazima basi hofu za aina hii zivunjwevunjwe kwa kujipa moyo kwamba hakuna chochote kisichowezekana katika maisha ya mwanadamu, kinachohitajika ni juhudi na maarifa na kuwa mvumilivu.
Kuongeza Ujuzi Na Maarifa
Hofu pia inaweza kutokana na ujinga au kutokujua. Kama mtu hana taarifa za kutosha kuhusiana na jambo analotaka kulifanya, anaweza kuwa na hofu na jambo hilo. Kwa hiyo, kinachotakiwa ni kukusanya taarifa na kujifunza zaidi juu ya jambo lenyewe kabla hajalianza.

Kwa mfano, kama mtu hajawahi kuendesha gari, anaweza akadhani kwamba kazi ya kuendesha gari ni ngumu sana. Kila anavyofikiria magari yanavyopishana njiani, ajali na vingine vingi, hofu yake huzidi kuongezeka. Lakini pale mtu anapoamua kuendesha gari na kuzoea kazi hiyo, hofu yote hutoweka.

Hivyo ndivyo ilivyo hata kwenye biashara. Kama kuna biashara ambayo mtu anataka kuifanya, lakini akawa haifahamu kiundani, anaweza akadhani biashara hiyo ni ngumu sana, lakini akiamua tu kuianza na kuizoea biashara yake, hofu inatoweka pia.
Kwa hiyo, suala zima la kujifunza na kukusanya taarifa, ni njia mojawapo inayomwondolea hofu mtu. Kadri mtu anavyoongeza ujuzi na maarifa katika jambo fulani, ndivyo anavyoweza kujaribu mambo mengi zaidi na kwa kujiamini.
‪#‎Kujifunza‬ kutoka kwa waliofanikiwa
Njia nyingine ya kuondoa hofu ni kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa. Mtu akiyapitia maisha ya wote waliofanikiwa, atabaini kwamba katika safari yao ya mafanikio, watu hao wamepitia vikwazo na changamoto nyingi sana.

Hata hivyo, licha ya vikwazo na changamoto zote hizo, atabaini kwamba waliweza kung’ang’ana hadi wakayafikia malengo yao. Hapo ndipo mtu anapaswa kujiuliza lile swali lililozoeleka miongoni mwa jamii yetu, la kwamba kama wao waliweza, kwa nini mimi nishindwe? Hii itasaidia kuondoa hofu!
Tunaishi kwenye dunia ambayo mtu anaweza kupata taarifa yoyote kwa urahisi, pale pale alipo. Hata kama mtu hawezi kujifunza moja kwa moja kutoka kwa mtu aliyefanikiwa, lakini anaweza kusoma vitabu na maandiko mengine yanayoelezea maisha ya watu hao waliofanikiwa.

Kwa kufanya hivyo, mtua anayetaka kufanikiwa katika biashara zake, anaweza kukutana na mtu anayemhamasisha na hivyo kumwondolea hofu na kumpa hamasa ya kumwezesha kushinda hofu iliyokuwa ikimkwaza kuchukua hatua juu ya malengo yake.
Fanya kwa vitendo.
Njia ya mwisho na bora ya kukabiliana na hofu ni kuanza malengo na ndoto yake kwa vitendo. Anza hatua kwa hatua kwa kujifunza hata kama kuna makosa yanatendeka. Fanya tathimini ya mara kwa mara ya kule ulikotoka na hapo ulipo ili tahimini hiyo ikujengee msingi imara wa kule unakotaka kufika.

Punguza maneno mengi katika kupanga. Hata kama mtu ana mipango mikubwa kiasi gani au akawa na mawazo mazuri kiasi gani, kama hachukui hatua ya kuanza kufanyia kazi mipango hiyo na mawazo hayo na madala yake akakalia maneno matupu, hakuna kitakachobadilika kwenye maisha yake.



Duniani kote, wote waliozingaia mambo hayo matano katika kukabiliana na hofu katika kila jambo wanalotaka kufanya kwa ajili ya kufikia mafanikio wanayoyataka, walifanikiwa.
Rais wa zamani wa Marekani, Franklin D. Roosevelt aliwahi kunukuliwa akisema: “Kitu pekee ambacho mtu anaweza akakihofia, ni hofu yenyewe.” Kauli hii inapaswa kuwa mwongozo kamili wa yeyote anayetaka kukabiliana na hofu kila anapopatwa na hofu fulani.
Kwa mawasiliano piga: +255 783 149 561 WhatsApp

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!