Monday 22 December 2014

WAWILI WAUAWA KWA KIPIGO



WATU wawili wameuawa kwa kipigo wilayani Tarime mkoani Mara, akiwemo mwanamke, aitwaye Suzan Bhoke (34), raia wa Kenya aliyekuwa akiishi kimapenzi na Eddy Clement, mkazi wa Kitongoji cha Forodhani katika mji mdogo wa Sirari.


Bhoke anadaiwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kusababisha kifo chake. Kutokana na kifo hicho, Clement alikamatwa na Polisi kwa msaada wa wananchi.
Mwingine aliyeuawa ni mkazi wa Kitongoji cha Turuturu Kijiji cha Nyakunguru kata ya Kibasuka, Marwa Burure aliyeuawa kwa kukatwa mapanga kichwani na sehemu mbalimbali za mwili na Chacha Matiko, aliyetoroka baada ya mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa alisema kuwa katika tukio la kwanza, Suzan Bhoke aliuawa na Eddy Clement anayedaiwa kuwa mpenzi wake kwa kile kilichodaiwa ugomvi wa wivu wa kimapenzi.
“Mtuhumiwa alimpiga na kitu kizito kichwani, hali iliyosababisha marehemu kuanguka na kukimbizwa hospitalini kupatiwa matibabu hospitali ya Migori nchini Kenya ambapo marehemu alifariki wakati akipatiwa matibabu,” alisema Kamanda Mambosasa.
Alisema Clement alikamatwa na wananchi wakishirikiana na askari na polisi, wanahoji na kisha watamfikisha mahakamani kujibu shitaka la mauaji ya Bhoke.
Mwili wa Bhoke ulifanyiwa uchunguzi na kuchukuliwa na ndugu zake kwa maziko. Kuhusu tukio la pili, Mambosasa alisema Marwa Burure aliuawa Desemba 19 saa 2.30 katika Kitongoji cha Turuturu kijiji cha Nyakunguru maeneo ya machimbo ya dhahabu ya Itandura. Alisema Burure inadaiwa aliuawa na Chacha Matiko.
Alisema polisi wanaendelea kumtafuta Matiko na aliomba wananchi kutoa ushirikiano ili kukamata mtu huyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!