Thursday 18 December 2014

TANZANIA KUUZA UMEME WA NCHI IFIKAPO MWAKA 2016


Tanzania inakusudia kuzalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya Watanzania wote na ziada kwa ajili ya kuunza nje ya nchi ifikapo mwaka 2016.



Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Felchesmi Mramba, aliyasema hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi wa shirika hilo nchini unaofanyika kwa siku mbili jijini Mbeya.

Alisema kuwa Tanesco imeanza ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi katika eneo la Kinyerezi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya nchi pamoja na ziada.

Alisema tayari awamu ya kwanza na ya pili ya mradi huo (Kinyerezi One na Two) yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 350 za umeme, imekamilika kwa asilimia 90 na inatarajiwa kuanza kazi ifikapo Machi, mwakani. 

Alisema awamu ya tatu na ya nne zitajengwa kwa ubia na Kampuni ya Kichina, ambapo katika awamu ya tatu Kampuni ya Kichina itamiliki asilimia 60 ya hisa na Tanesco itamiliki asilimia 40, huku awamu ya nne ambayo itakuwa na mtambo wa kuzalisha megawati 600 za umeme, Tanesco itam6iliki asilimia 30 na kampuni ya Kichina itamiliki asilimia 70.

Kwa mujibu wa Mramba, miradi hiyo yote itarajiwa kukamilika na kuanza kufanya kazi ifikapo mwaka 2016, hali ambayo italifanya tatizo la kukatika katika kwa umeme nchini kubaki historia.

Alisema katika mikakati ya kuuza ziada ya umeme nje ya nchi, tayari Tanesco imesaini mkataba wa kujenga njia kubwa ya kusambaza umeme kwa nchi tatu za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuuziana umeme wa ziada.

Alisema sehemu ya kwanza ya ujenzi wa njia hiyo itakuwa ni kuanzia Nairobi nchini Kenya hadi Singida na awamu ya pili itaanzia Iringa kuelekea Dodoma, njia ambayo itaendelezwa hadi mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Hata hivyo, wakati shirika hilo likitangaza mikakati hiyo mizuri yenye matumaini kwa Watanzania, mgeni rasmi kwenye mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, kupitia katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Profesa Norman Sigalla, alisema kuwa Tanesco haitaeleweka kirahisi kwa wananchi kama mikakati hiyo haitatekelezwa kwa vitendo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!