Saturday 20 December 2014

IPTL, PAP ZAPINGA BUNGE MAHAKAMANI



KAMPUNI za Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP) na Independent Power Tanzania Ltd (IPTL) na Harbinder Singh Sethi, wamefungua kesi ya kikatiba kupinga utekelezaji wa maazimio ya Bunge yaliyotolewa kuhusu sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inayodaiwa kuchotwa zaidi ya Sh bilioni 300.



Kesi hiyo ilifunguliwa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya hati ya dharura dhidi ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Ilifunguliwa kupitia mawakili watatu wa kampuni hizo, ambao ni Joseph Makandege, Melchsedeck Lutema na Gabriel Mnyele.
Mawakili hao wanadai kwamba uamuzi uliotolewa na Bunge, uliegemea upande mmoja kwa vile baadhi ya wahusika walioshiriki, ikiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila wana kesi kuhusu sakata hilo.
Pia, walidai kilichofanyika ndani ya Bunge kuhusu sakata hilo ni kinyume cha Katiba kwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria alitafsiri vibaya amri halali, iliyotolewa na Mahakama ya kuzuia mjadala huo usijadiliwe bungeni.
Mawakili hao walidai kwamba mahakama ilikusudia Bunge liweze kuendelea na shughuli zake za kawaida wakati shughuli nyingine zinazohusu maombi hayo zikitekelezwa.
Miongoni mwa maazimio yaliyowasilishwa bungeni ni kwamba Sethi, James Rugemalira, Waziri wa Nishati na Madini na Katibu Mkuu wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), walihusika kufanya miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow kwenda kwa makampuni ya PAP na VIP Engineering & Marketing.
Bunge liliazimia kwamba Takukuru, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama, viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi, watu wote waliotajwa na Taarifa Maalum ya Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusu miamala ya Akaunti ya Escrow.
Pia, bunge lilisema kutokana na vitendo vya kijinai wanavyohusishwa navyo viongozi wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini, vinakiuka maadili na kuwanyima viongozi na maofisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma wa kuwawajibisha kwa kuishauri.
Hivyo azimio la pili Bunge liliwataka viongozi hao akiwemo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao.
Katika azimio la tatu, Bunge liliazimia kwamba Kamati za Bunge zichukue hatua za haraka, kwa vyovyote kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao Wenyeviti tajwa wa Kamati husika za Kudumu za Bunge; Pia, azimio la nne, Bunge lilimtaka Rais Jakaya Kikwete aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi, kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambao wanahusishwa katika kashfa hiyo.
Maazimio mengine yaliyotolewa na Bunge kuhusu sakata hilo ni mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi, ziitaje Stanbic Bank Ltd na benki nyingine zitakazogundulika, kufuatia uchunguzi uliofanywa na mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
Hata hivyo, Bunge liliitaka Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya Sheria iliyoiunda Takukuru kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa; Vile vile, Bunge liliaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!