Thursday 30 October 2014

TIGO NA FACEBOOK KUTOA HUDUMA ZA INTERNET BURE KUPITIA INTERNET.ORG

2
- Inatarajia kuongeza idadi ya watumiaji wa intenet nchini 
- Upatikanaji wa intanet kupitia simu za ‘smartphone’ za bei nafuu kutoka Tigo

Tigo jana imetangaza kwamba watashirikiana na kampuni ya mtandao wa kijamii Facebook kuwapatia mamilioni ya Watanzania huduma ya intanet kwa bei nafuu kupitia ‘application’ maalum ya Internet.org.
Tigo pia inatoa fursa ya wateja kununua na kumiliki simu za kisasa ‘smartphones’ kwa bei nafuu, kuwapatia huduma bora ya intanet na kutoa huduma ya bure kabisa kwa tovuti zinazohusiana na elimu, afya, habari na mitandao ya kijamii kupitia Internet.org.
App ya Internet.org itaanza kutumika kuanzia 29 Oktoba na itawapatia wateja wa Tigo fursa ya kutumia tovuti na apps kama: AccuWeather; BabyCenter & MAMA; BBC News & BBC Swahili; BrighterMonday; The Citizen; Facebook; Facts for Life; The Girl Effect; Messenger; Mwananchi; Mwanaspoti; OLX; Shule Direct; SuperSport; Tanzania Today and Wikipedia.
Akizungumzia kuhusu uzinduzi wa huduma hizo leo, Mkuu wa Idara ya Data na Vifaa vinavyotumia Intanet, David Zacharia, alisema, “Kupitia ushirikiano huu na Facebook tunadhamiria kuongeza wigo wa matumizi ya kidijitali nchini kwa kuwahamasisha Watanzania wengi zaidi kuingia mtandaoni.”
Zacharia aliendelea kusema kwamba ushirikiano huo kati ya Tigo na Facebook itazidi kuendeleza matumizi ya intanet nchini lakini pia itasaidia kufungua milango mipya ya fursa za kiuchumi na kijamii kwa walio katika sekta mbali mbali za elimu, teknolojia, sanaa na biashara.
Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaeleza kwamba watumiaji wa intanet nchini Tanzania imeongezeka kutoka milioni 7.5 mwaka 2012 mpaka milioni 9.3 mwezi wa Juni 2014 ambayo ni sawa sawa na ongezeko la asilimia 18.
Tigo, kupitia mmiliki wake Millicom, tayari wana ushirikiano na Facebook nchini Tanzania na Paraguay ambayo inawapatia wateja wake matumizi ya bure kabisa katika mtandao huo wa kijamii.
“Leo tunapanua ushirikiano wetu na Tigo nchini Tanzania kutoka katika kutoa huduma za bure kupitia mtandao wetu wa Facebook na kujumuisha huduma za kupata taarifa muhimu kwenye sekta ya afya, elimu, mawasiliano, uchumi, ajira na habari za kitaifa. Kwa kuwapatia Watanzania teknolojia na huduma hizo kwa gharama nafuu tunaamini ya kwamba tunaweza tukaharakisha mchakato wa kuwaunganisha kila mtu katika ulimwengu wa intanet na dijitali,” alisema Meneja Bidhaa wa Internet.org kutoka Facebook, Andrew Bocking.
Wateja wa Tigo nchini wanaweza wakapata app ya Internet.org kupitia huduma ya Google Play Store, kwa kutembelea www.internet.org kupitia simu zao za mkononi, kupitia ‘Tigo Portal’ na pia kupitia ‘bookmark’ iliyopo katika huduma ya kuperuzi ya Opera Mini. Huduma hii inaweza ikatumika kupitia simu za kisasa ‘smartphones’ au simu za kawaida pia.
Internet.org ni mpango maalum uliobuniwa na Facebook yenye lengo la kuwapatia huduma za intanet yenye gharama nafuu kwa theluti tatu ya watu duniani ambao bado hawajaunganishwa na intanet ili kuweza kuwapatia fursa zile zile ambazo theluthi ya watu duniani iliyobaki wanaendelea kupata.    
App ya Internet.org inafanya mtandao wa intanet kuwafikia watu wengi zaidi kupitia kundi la huduma za bure ambazo zinawezesha watu kuperuzi taarifa na tovuti mbali mbali zenye msaada kwao bila kuingia gharama yeyote.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!