Friday 24 October 2014

MADAKTARI WA TANZANIA WALIOKWENDA KUKABILIANA NA EBOLA AFRIKA MAGHARIBI

Unaposikia ugonjwa wa ebola, ni sawa na kusikia sauti ya mauti. Ugonjwa huu ambao unaliandama eneo la Afrika Magharibi umesababisha vifo vya maelfu ya watu na hata kuuingiza ulimwengu kwenye wasiwasi mkubwa.

Ugonjwa huu huweza kuambukizwa kwa kugusana tu, kwa kuwa virusi vinavyoeneza maradhi haya huishi katika majimaji ya mwilini yakiwamo mate, damu na hata jasho.
Pamoja na hatari ya ebola, lakini Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa maagizo ya Rais Jakaya Kikwete, ilituma timu ya madaktari bingwa watano kwenda katika nchi zilizoathirika na ebola ili kusaidia.
Madaktari hao ni Justin Maeda ambaye ni mganga mkuu wa Hospitali ya Mvomero, mkoani Morogoro, Theopili Malibicha kutoka Hospitali ya Mkoa wa Lindi, Godbles Lucas, wizarani, Erild Temba kutoka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na Saasita Ramadhan kutoka Chunya, Mbeya.
Madaktari wote hawatakwenda eneo moja. Dk Maeda, Malibicha na Lucas wataenda Liberia, wakati Temba na Ramadhan wakienda Sierra Leone.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja anasema madaktari hao wamekwenda katika nchi hizo ili kusaidia kutoa huduma za afya na kupata ujuzi.
“Kitendo cha madaktari hawa kwenda katika nchi zenye ebola si cha kutisha kama wengi wanavyodhani kwani ni sawa na askari anayekwenda vitani,” anasema.
Anasema mwanajeshi hupata mafunzo akijua siku yeyote anaweza kupata wajibu wa kwenda kupigana kwenye vita ambako kuna kufa au kupona.
Jarida la Forbes linaeleza kuwa hadi sasa ebola imeua wahudumu wa afya zaidi ya 230.
“Kumhudumia mgonjwa wa ebola ni kazi ngumu na ni rahisi kuambukizwa wakati mgonjwa anapokuwa katika hali mahututi,” anasema Dk Innocent Mosha wa Kitengo cha uchunguzi wa magonjwa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa watu zaidi ya 4,000 wamefariki kwa ugonjwa huo hadi sasa. WHO inaeleza zaidi kuwa endapo hatua stahiki hazitachukuliwa, ugonjwa huo unaweza kusababisha vifo zaidi.
Mmoja wa madaktari hao, Justin Maeda ambaye timu yake ipo Liberia, anasema kwa sasa wapo katika mafunzo ya usalama kazini ambayo yatawawezesha kujilinda wenyewe na kuwalinda wote wanaowazunguka.
“Tupo salama sana, nawataka Watanzania wasiwe na wasiwasi kwa sababu taratibu zote zimechukuliwa na kuzifuata siyo ombi ni lazima.
“Wapo watu ambao wameajiriwa, kazi yao kutufuatilia na kuhakikisha kuwa tunafuata njia zote za kulinda usalama wako binafsi na wale wanaokuzunguka,” anasema Dk Maeda.
Dk Maeda anasema timu ya Liberia tayari imeungana na timu nyingine za mashirika ya kimataifa na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC) kwa ajili ya kujaza mapengo yaliyopo hasa katika mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa.
Anasema, wataalamu wa afya wanaohudumia wagonjwa wa ebola hawatakiwi kuacha wazi sehemu yoyote ya mwili.
“Wagonjwa wote wa ebola katika karantini wanatakiwa kuonwa na meneja wa eneo kila wakati na katika kila hatua,” anasema.
Vifaa vya kujikinga kwa mhudumu wa afya huzingatiwa ili kuzuia maambukizi kwa sababu ebola huambukizwa kwa njia za moja kwa moja kwa mfano ngozi iliyo wazi au maji maji na ute wa machoni, puani na mdomoni.
Damu au majimaji ya mwilini ya mtu mwenye ebola pamoja na vifaa vilivyotumiwa na mtu mwenye ebola kama sindano na mikasi.
Madaktari wanaofanya kazi katika nchi zilizoathirika na ugonjwa huo, wanawekwa katika mazingira ya uangalizi wa hali ya juu, kuhakikisha usalama.
Kwa mfano madaktari hutakiwa kumtambua na kumtenga mgonjwa aliyegundulika na kumuweka katika chumba cha pekee, ambacho hutakiwa kufungwa milango.
Pia mgonjwa huyo atumie bafu na choo chake mwenyewe.
Kituo cha CDC pamoja na WHO kimetoa miongozo mingine ambayo ni kupunguza idadi ya wahudumu wa afya wanaomuhudumia mgonjwa wa ebola.
WHO inasema ni vyema mtaalamu mmoja wa afya akawa na zamu ya muda mrefu ili mgonjwa asihudumiwe na madaktari wengi. Hii itapunguza maambukizi kwa wataalamu wa afya.
Madaktari hao wanaeleza kuwa tahadhari nyingine ni kuepuka kujishika usoni kupunguza uwezekano wa kushika majimaji ya mwili pamoja na kujizuia kushika vitu vyenye ncha kali.
Tahadhari nyingine ni matumizi mazuri ya ‘gloves’ zenye dawa mara baada ya kumshika mgonjwa.
Vile vile eneo alilokaa au kulala mgonjwa wa ebola hutakiwa kuoshwa vyema kwa dawa maalum kabla ya kutumiwa kwa shughuli nyingine yeyote.
“Katika kesi nyingi tumepewa mafunzo kuwa tutumie ‘gloves’ mbili badala ya moja” anasema.
Hali ya ebola kidunia
Nchini Guinea, kwa sasa inakisiwa kuwa watu 1519 walioambukizwa ugonjwa huo, lakini walithibitishwa kwa vipimo vya kimaabara ni 1,217 na waliokufa ni 862.
Liberia wameambukizwa watu 4,249 na waliokufa ni 2,484 wakati nchini Siera Leone kuna matukio 3,410 ya walioambukizwa lakini waliothibitishwa kwa vipimo vya kimaabara ni 2,977 na vifo ni 1,200. Ugonjwa huo umekuwa ukienea kwa kasi katika nchi tatu za Afrika Magharibi kwa wale wanaomsaidia mgonjwa bila kuwa na tahadhari, wauguzi na kwa wanajamii wanaoandaa mwili kwa mazishi. Wengi wa watu walioupata ugonjwa huo nje ya bara la Afrika ni wale ambao walitoa huduma za kuwasaidia wagonjwa.
Ebola Tanzania
Hapa nchini mpaka sasa hakuna mtu aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo ingawa tayari Serikali imetenga vituo maalumu kwa tahadhari iwapo atapatikana mgonjwa wa namna hiyo.
Hata hivyo, hali inayoashiria kuwa Watanzania wako kwenye hali ya tahadhari, wamekuwa makini kuhakikisha wanaripoti haraka wanapoona mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Hadi wiki hii, kulikuwa na wagonjwa wawili wakihofiwa wana ebola, lakini baadaye taarifa zilithibitisha kuwa walikuwa na magonjwa mengine.
Tukio la kwanza ni la mgonjwa wa Wilaya ya Nkasi, mkoa wa Rukwa na la pili ni mgonjwa aliyefariki huko katika kijiji cha Kahunda wilayani Sengerema.
Tiba ya ebola
Ebola kama ilivyo maradhi mengine yanayosababishwa na virusi, umekuwa ukiwapa wakati mgumu wanasayansi katika kupata kinga au tiba.
Zipo chanjo kadhaa ambazo tayari zipo kwenye hatua ya majaribio maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, virusi vya ebola kama vilivyo vile vya Ukimwi, huweza kujibadilisha ghafla hivyo kuwa ni vigumu kutibiwa na dawa fulani.
Mpaka sasa tiba na chanjo zilizofanyiwa utafiti na kuonyesha matumaini ni pamoja na tiba ya ZMapp iliyofanyiwa utafiti na kampuni ya Mapp Biopharmaceutical, dawa za tekmira zilizotengenezwa na kampuni ya Tekmira Pharmaceuticals nchini Canada na TKM-Ebola ambayo imetengenezwa kuviua virusi vya ugonjwa huo.
Dawa nyingine ni ile iliyotengenezwa na kampuni ya Kimarekani ya Sarepta ambayo imefanyiwa majaribio kwa binadamu kwa kujitolea kama sehemu ya majaribio.
Dawa ya ZMapp iliweza kuwatibu madaktari wawili wa Marekani ambao waliambukizwa wakiwa katika harakati za kuwasaidia wagonjwa Afrika Magharibi.
WHO inasema majibu kamili ya majaribio hayo yatafahamika mwakani.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!