Friday 24 October 2014

KUCHAPA WATOTO HUATHIRI AFYA NA UWEZO WAO KIAKILI

Je, mwanafunzi anachapwa viboko ili kumjenga kitabia au kumuathiri uwezo wake wa kumudu elimu anayopatiwa?
Kuna sababu nyingi za kimila, kitamaduni na za kidini zinazosababisha watu wazima kuwapiga watoto kama njia ya kuwaweka katika mstari wa kimaadili.
Katika nchi nyingi duniani, watoto wengi hupigwa au kuchapwa na wazazi, walezi na waalimu kama njia ya kuwaadibisha ili waone maumivu yatakayowaogopesha wasirudie makosa.
Kwa mujibu wa utafiti wa kitaifa kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto nchini Tanzania uliofanyika mwaka 2009, asilimia 73.5 ya watoto wa kike na 71.7 wa kiume hapa nchini, hukabiliwa na ukatili ambao kwa kiasi kikubwa unahusisha vipigo vya aina mbalimbali.
Wazazi wengine huwapa watoto wao vipigo vilivyopitiliza ambavyo vyaweza kutafsiriwa kuwa si njia ya kumkanya mtoto, bali ni kumnyanyasa kinyume na haki za binadamu.
Watoto wengine hutendewa ukatili kama vile kuchomwa kwa moto sehemu mbalimbali za miili yao kwa kisingizio cha kuwarekebisha tabia.
Wanasayansi wanaeleza kuwa kitendo cha kuwapiga watoto kinaweza kuwasababishia madhara makubwa ya kiafya katika kipindi cha utoto wao na hata watakapofikia umri wa utu uzima.
Kipigo kwa mtoto kinaweza kuathiri afya ya mwili na akili pia. Utafiti ulioongozwa na Eamon McCrory wa Chuo Kikuu cha London ulibaini kuwa kuwachapa au kuwapiga watoto kunaathiri utendaji wa ubongo.
Katika utafiti mwingine, ilibainika kuwa kwa kadri mtoto anavyopata vipigo na kuumia kisaikolojia, ndivyo seli za sehemu mbalimbali za ubongo wake zinavyopungua.
Hali hii hupunguza uwezo wa kiakili wa mtoto na wakati mwingine humsababishia athari za kisaikolojia.
Wengi hujenga tabia ya ukatili kwa wenzao na kupoteza moyo wa huruma. Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa Lopez N na wenzake uliochapishwa kwenye jarida la North America Journal of Psychology toleo la 3 la mwaka 2001.
Naye, Rosalind Downing, ambaye ni daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika Hospitali ya Advocate Good Samaritan nchini Marekani, anasema: “Kipigo huwapatia watoto ujumbe mbaya unaoonyesha kuwa ukali na kipigo ndiyo njia inayofaa katika utatuzi wa matatizo maishani.”
Utafiti wa Ulman A na Straus M.A wa mwaka 2003 uliochapishwa katika jarida la maswala ya kifamilia lijulikanalo kama Journal of Comperative Family Studies, toleo la 34, nao ulibaini kuwa watoto wanaopata kipigo mara kwa mara hujenga chuki mbaya dhidi ya wazazi, walezi au walimu wao na kutokupenda kukaa nao.
Hii huwafanya wawachukulie kama maadui na watu wasio wema kwa maisha yao.
Katika utafiti uliofanywa na Shirika la Mkombozi mkoani Kilimanjaro na Arusha, 2007 uliwahusisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu mitaani.
Katika utafiti huo ilibainika kuwa asilimia 53 ya vijana hao kabla ya kukimbia familia zao na kwenda mitaani, walitendewa vitendo vyenye uwezo wa kudhuru afya ya mwili.
Asilimia 61 walidai kuwa walipigwa, wakapata majeraha na kuumizwa mara kwa mara na watu waliokuwa wanakaa nao kama wazazi au walezi.
Watafiti wengi wa masuala ya afya ya jamii, wanasema kuwa watoto wa namna hii hukabiliwa na msongo mkali wa mawazo, huwa na tabia ya ukali, tabia ya kutojithamini, matumizi ya dawa za kulevya na pia hukabiliwa na tabia ya kupenda kujiua.
Hyland na wenzake katika utafiti wao uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Journal of Behavioral Medicine la Septemba 29, 2012, walibaini kuwa kipigo cha mara kwa mara kwa watoto kinaweza kusababisha magonjwa sugu kama vile saratani pumu na magonjwa ya moyo.
Ni vyema kuwapa watoto adhabu zisizohusiana na kipigo pale wanapokosea. Ni vyema pia, kuwaelekeza kwa maneno na kuwaonyesha makosa yao kwa upendo bila hasira.
Maelekezo ni vyema yakaandamana na hali ya kuwaonyesha unawapenda ila unachukia makosa yao.
Njia hii inaweza kuwa bora zaidi katika kuwafundisha watoto uwajibikaji na kuepuka makosa kwani inawajengea kujiamini.
Pale inapokuwa lazima kutumia kiboko, basi tahadhari ichukuliwe ili kuepuka madhara ya afya ya mwili yanayoweza kutokea au kuwasababishia hofu kali.
Ikumbukwe kuwa lengo la adhabu ni kumjengea mtoto maadili mema na siyo kumuumiza na kumjengea moyo wa chuki, msongo wa mawazo na kumsababishia magonjwa ya akili.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!