Tuesday 21 October 2014

KARAFUU YA ZANZIBAR YAZIDI KUTESA SOKO LA DUNIA


MSHAURI wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Sadruddin Govinji amesema karafuu ya Zanzibar imeendelea kupata umaarufu katika soko la dunia kutokana na sifa zake za kipekee zenye ubora.



Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa majukumu kwa Kamati ya Fedha, Kilimo na Biashara ya Baraza la Wawakilishi (BLW), Zanzibar katika Tawi la ZSTC lililopo ‘Al-Qusais Industrial Area’ Dubai, mshauri huyo alisema wananchi wa Dubai na wengineo kutoka katika sehemu tofauti wanaotembelea nchi hiyo kibiashara wamekuwa wakivutiwa sana na kununua karafuu ya Zanzibar ukilinganisha na karafuu kutoka nchi nyingine.
Alisema hatua ya ZSTC kuweka karafuu za vifungashio vya ujazo mdogo imewavutia wateja wengi kwa vile ni rahisi kwa wananchi kununua karafuu hizo katika ujazo wanaouhitaji. Aliongeza ujazo huo mdogo wa kilo moja, nusu na robo kilo kutokana na ulivyosanifiwa, umekubalika sana Dubai na unachukua nafasi ya pili kukubalika miongoni mwa viungo vinavyouzwa nchini humo.
Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji ya ofisi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mwendeshaji, Naibu Mkurugenzi wa Fedha, Ali Suleiman alisema ZSTC ilifungua ofisi hiyo mwaka 1993 kwa madhumuni ya kuwa kituo cha shirika katika kutangaza zao la karafuu ya Zanzibar kwa nchi za Falme za Kiarabu.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo ya Fedha, Kilimo na Biashara, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Salmin Awadh Salmin, alisifu jitihada za ZSTC za kuliimarisha zao la karafuu na kuchukua juhudi za kuzitafutia soko kupitia tawi hilo la Dubai.
Naye Ofisa Mwandamizi wa Ubalozi Mdogo wa Dubai, Clephas Kaseza Ruhumbika alilishauri Shirika la ZSTC kuongeza uzalishaji wa karafuu ili kukidhi mahitaji ya zao hilo katika soko la dunia.
Aidha Ruhumbika aliishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano kuchukua jitihada za ziada kuwaelimisha vijana kutambua fursa na uzalishaji na ajira zilizopo ndani ya nchi badala ya kuwaacha wakihangaika kutafuta kazi nje ya nchi.

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!