Tuesday 30 September 2014

MILIONEA MAARUFU WA JWTZ ALIVYOUWA KINYAMA KWA RISASI

Stori: Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’
NI taharuki iliyojaa majonzi na simanzi kufuatia Jeshi la Wananchi wa Tanzania ‘JWTZ’ Kikosi cha CMTU jijini Dar kuondokewa na mpiganaji wake, Sajenti Yohana  Lugendo Gweso (40) ambaye alikuwa milionea aliyepigwa risasi sita mwilini na kufariki dunia papo hapo.
Mwili wa marehemu Sajenti Yohana Lugendo Gweso (40) wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ‘JWTZ’ Kikosi cha CMTU ukiwa kwenye jeneza.

Tukio hilo la kusikitisha, lilijiri saa 1:45 usiku wa Septemba 22, mwaka huu, Ukonga Babana ndani ya baa maarufu ijulikanayo kwa jina la Super Karatu.
UWAZI HATUA KWA HATUA
Kufuatia tukio hilo, Uwazi kama kawaida yake lilifuatilia kwa kina ili kubaini yaliyofichika nyuma ya pazia kama siyo sirini!
Gari kubwa la jeshi lililoandaliwa kwa ajili ya kuuchukua mwili wa marehemu Sajenti Yohana  Lugendo Gweso kwenda Bunda kwa mazishi.
Habari zilizopatikana zilidai kuwa, siku ya tukio, marehemu Gweso alipigiwa simu akiwa njiani kurudi nyumbani kwake akitokea Hospitali ya Dar Group iliyoko Tazara jijini Dar.
Ikadaiwa kuwa, baada ya kupata simu hiyo alifika kwanza nyumbani kwake Gongo la Mboto kambini.
“Alipofika alikula chakula cha mchana kisha alipumzika. Ilipofika saa 11 jioni aliondoka kwenda kwenye shughuli zake za biashara. “Alipokuwa huko inadaiwa alipigiwa simu na mtu huyo wa mwanzo na kupanga sehemu ya kukutania ambapo ilikuwa  ni hapo baa,” alisema ndugu mmoja akiomba kusitiriwa jina lake.
Wanajeshi wa JWTZ wakiupandisha mwili wa Sajenti Yohana Lugendo Gweso kwenye gari.
AONDOKA NA NDUGU
Mpiganaji huyo inadaiwa wakati anatoka katika biashara zake alikuwa na mtoto wa dada yake aliyetajwa kwa jina moja la Frank ambaye alikuwa akisimamia hesebu zote za biashara. Siku hiyo walikuwa wamekusanya kiasi cha shilingi milioni 42.
Ikadaiwa kuwa, walipofika Banana kabla ya kuingia Baa ya Super Karatu, marehemu ambaye alikuwa akiendesha gari lake aina ya Toyota Prado lenye namba za usajili T 855 BWK, alimshusha Frank na kumtaka atangulie  nyumbani kwani alihitaji kwenda Super Karatu kukutana na mwanamke huyo ambaye baadhi ya watu wanadai ni mweupe, mnene aliyepanda hewani (mrefu).
Mjane (mwenye kilemba cheupe) wa marehemu Sajenti Yohana  Lugendo Gweso akisaidiwa na ndugu wa karibu kuingia kwenye gari lililoandaliwa kwa ajili ya safari.
AFIKA ENEO LA MAUAJI YAKE
Habari zaidi zinasema kuwa, marehemu aliwasili kwenye baa hiyo saa 1 usiku na kutafuta  maegesho. Alishuka na kuanza kutembea, lakini ghafla kwa  nyuma aliitwa na watu wawili ambao walimuita; “Gweso tuko hapa.”
Wakati anageuka kuwafuata watu hao, watu wengine walianza kuvunja gari lake vioo hivyo alirudi mbio ili kujua nini kinaendelea.
“Kumbe wau hao walikuwa kundi moja na mashambulizi ya risasi yalianzia hapo.
“Marehemu alimiminiwa risasi sita mwilini, alipigwa kichwani, nyingine kifuani na walimchukulia fedha zote milioni 42 na bastola yake kisha wakatokomea,” aliendelea kusema ndugu huyo.
Waombolezaji wakiingia kwenye gari kuelekea kwenye mazishi, Bunda.
MWILI WAKUTWA CHINI
Baada ya tuko hilo ndugu, jamaa na marafiki walijulishwa kuhusiana na kifo cha mjeshi huyo ambapo walifika na kuuchukua  mwili wa marehemu hadi Hospitali ya Rufaa ya Lugalo jijini Dar kwa ajili ya kuuhifadhi.
UTAJIRI WA MAREHEMU
Mpaka kifo chake, marehemu Gweso alikuwa akimiliki magari manne ya kisasa, Toyota Prado (alikuwa nalo siku ya tukio), Toyota Verossa, Suzuki Vitara na VRS.
Aidha, alikuwa akimiliki biashara mbalimbali kama vile baa, duka la bia za jumla na nyumba ya kulala wageni. Vyote vipo Ukonga, Dar.
Waombolezaji wakiuchukua mwili wa Sajenti Yohana  Lugendo Gweso kwa ajili ya mazishi.
Baadhi ya waombolezaji siku ya msiba walimtaja marehemu kuwa mwanajeshi milionea aliyehakikisha anapiga hatua kwa biashara kila kukicha.
ALIANZA KUWINDWA MWAKA 2008
Habari zaidi zinadai kuwa, marehemu alianza kuwindwa mwaka 2008 ambapo watu wasiojulikana majina, sura wala nia yao, walivamia nyumbani kwake, Banana (uswahilini) na kumpiga risasi mtoto wa dada yake na kufariki dunia papo hapo.
Sajenti Yohana  Lugendo Gweso enzi za uhai wake.
Inadaiwa watu hao waliamini mtoto huyo ni Gweso mwenyewe lakni yeye hakuwepo. Kufuatia tukio hilo, marehemu aliomba kuhamia kambini kwa usalama wake hadi kifo kilipomkuta hivi karibuni.
MAZISHI YAKE
Marehemu Gweso amezikwa Septemba 27,  mwaka huu katika Makaburi ya Kijiji cha Tailo Wilaya ya Bunda Mkoani Mara. Ameacha mke mmoja na watoto wanne.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!