Friday 22 August 2014

TUKO DODOMA KULA POSHO TU!-MJUMBE

Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Alli Omari Juma amefuta matumaini ya Watanzania kuhusu kupatikana kwa Katiba mpya, badala yake akabainisha kuwa wajumbe wako Dodoma kwa ajili ya kula posho tu.

“Nawakumbusha watu kufuta matumaini ya kupata Katiba Mpya, kinachojadiliwa hapa ni mambo ya kulazimishana kila upande, sisi wengine tunaona bora ya Ukawa waliotoka nje kuliko mambo ya humu ndani,” alisema Juma na kuongeza:
“..Hata wale Wapemba waliokwenda Umoja wa Mataifa kudai haki ya kujitenga , naona walikuwa halali kwani hapa bungeni hakuna mwakilishi hata mmoja kutoka huko wakati tunaambiwa kuwa itakuwa Katiba ya wote, ni kudanganyana.”
Mjumbe huyo alisema kuwa Rasimu ya Warioba imetupwa na wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi kiasi cha kuwafanya wengine waone kuwa kinachotengenezwa ni marekebisho ya Katiba ya 1977.
Alisema kuwa suala la akidi pia litakuwa ni moja ya vikwazo vitakavyosababisha kutopatikana kwa Katiba, akitolea mfano kutoka kwenye kamati yake Namba 4.
Alisema ndani ya kamati hiyo mambo mengi yanachakachuliwa kwani wajumbe wanaotakiwa kutoka Zanzibar ni 14 lakini waliopo ni 12 tu, ambao baadhi hawakubaliani na mawazo ya CCM lakini wanaambiwa mambo ni mazuri.
“Ukawa walitoka kwa uhalali kabisa nami nawaunga mkono, sisi tuliobaki humu ndani tulikuja kwa makusudi ya kuangalia kinachoendelea na sasa tunaona mambo ni ovyo,” alisema.
Kwa upande mwingine alimlaumu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu Samuel Sitta kwamba amekuwa ni kinara wa kuvuruga kanuni kila wakati na kutaka mambo yake mwenyewe.
Jumba ambaye ni mtaalamu wa sheria, aliwatupia lawama pia viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwamba nao wanapaswa kulaumiwa kwa kushindwa kuwaweka Wazanzibar pamoja ili wajue wanataka nini.
Kwa mujibu wa Juma, kila maeneo wanayojadili wanafanya kazi hiyo kwa kuboresha maslahi ya CCM kwani wanawasaidia kuwaandikia Ilani yao.
Alimtaka rais Jakaya Kikwete kukubaliana na maoni ya watu mbalimbali kwamba bunge la Katiba lisitishwe mara moja kuliko kuendelea kujadili misimamo mikali ya CCM

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!