Saturday, 12 April 2014

MIRUNGI YA KIDONGE YATEKA MAMIA YA WATANZANIA

Unapolitaja neno ‘mirungi’ macho na hisia zako zitakupeleka katika dawa za kulevya zilizo katika mfumo wa majani au mimea ambazo ni maarufu Afrika Mashariki. Hapa nchini mirungi imeharamishwa kulingana na sheria ya dawa za kulevya.
Hata hivyo kwa sasa, mirungi hii haitumiwi ikiwa katika hali ya mimea tu kama ilivyozoeleka bali katika mfumo wa kidonge (kitaalamu synthetic cathinone) ambacho ni vigumu kufahamu kama ni mrungi.
Dawa hii ya kulevya ni maarufu na ina majina mengi hapa duniani, baadhi ya majina hayo ni miraa, khat kwa Kiingereza, ghat, qat, hagat, bushman tree (Afrika Kusini) na baadhi wanauita mmea huu Arabian.
Imebainika kuwa mirungi ya vidonge huingizwa nchini katika vifurushi vilivyobandikwa lebo kama vile dawa za kuua wadudu, bath salt, sumu kali, dawa za kusafishia vioo au simu na mimea.
Mwaka 1980, Shirika la Afya Duniani liliipanga mirungi kuwa katika kundi la dawa za kulevya na mihadarati inayosababisha utegemezi, wakati hapa nchini mirungi ilipigwa marufuku Aprili 1991.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili na mshauri wa watumiaji wa dawa za kulevya, Innocent Godman, alifanya utafiti mwaka 2004 kuhusu utumiaji wa mirungi hapa nchini, ambao ulibaini kuwa kuna ongezeko kubwa la watumiaji wa mirungi ya kidonge.
“Ingawa mirungi ya vidonge imeanza kutumika katika siku za karibuni, lakini mirungi ya mimea, ilianza kutumiwa miaka 800 iliyopita,” anasema Dk. Godman.
Mirungi ya kidonge inatajwa kuwa na madhara makubwa kuliko ile ya mimea, kwani husababisha mtumiaji kupata raha ya ngono au kilele cha mapenzi kwa sekunde 17 tofauti na hali ya kawaida ambapo binadamu hupata kilele hicho kwa sekunde tatu tu.
“Kidonge cha mirungi kimekuwa maarufu zaidi kwa sababu mtumiaji hupata raha ya mapenzi kwa muda mrefu na hivyo kumfanya asiwe na sababu ya kuwa na mwenza,” anasema na kuongeza:
“Mirungi hii ina kileo kinachoitwa ‘cathinone’ mbacho ni kichocheo kinachobadilisha kasi ya ufanisi wa ubongo. Kinasogeza mbele uchovu, njaa na kuongeza umakini. Kikubwa zaidi kileo hicho husababisha raha ya ngono (euphoria) kudumu kwa muda mrefu.”
Dk. Godman anasema, matumizi ya kidonge cha mirungi hapo zamani yalizoeleka zaidi kwa watu wazima wenye umri wa miaka 50 na kuendelea wenye matatizo ya nguvu za kiume, lakini hivi sasa, vijana wadogo wanatumia vidonge hivyo.
Katika utafiti huo ilibainika kuwa watumiaji wa mirungi hupenda kutembelea maeneo maalumu kwa mfano Dodoma, ni karibu na soko kuu na Arusha, ni maeneo ya Ngaramtoni, Makao Mapya na Kaloleni. Lakini yapo maeneo maarufu katika Jiji la Arusha na Dar es Salaam yanayoitwa Manjili Sairat ambayo yanasifika kwa kuuza mirungi ya majani na kidonge
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!